Saturday, 9 January 2016

Wasiopeleka Watoto Shule Kuburuzwa k=Kortini Machi 30

SERIKALI imesema haitosita kuwafungulia mashtaka na kuwapeleka mahakamani ifikapo Machi 30, mwaka huu, wazazi ama walezi wote watakaoshindwa kupeleka watoto wao shuleni ili kupata elimu ya msingi na sekondari.

Aidha, imepiga marufuku kwa jamii kutumia jina la ‘watoto wa majumbani’, badala yake waitwe wasaidizi hao ‘wasichana wa kazi’ au ‘vijana wa kazi’. Hayo yalisemwa na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu, Dar es Salaam jana.

Alisema hayo ili kuhamasisha wazazi na walezi juu ya watoto kujiunga na shule za msingi na sekondari kwa mwaka huu 2016.
Kuhusu kuwafungulia wazazi mashtaka, alisema serikali inaamini kuwa ikiwa inataka kujenga taifa lililoelimika ni lazima kuwekeza kwenye elimu, hivyo ni wajibu wa kila anayehusika kuhakikisha anatimiza wajibu wake.

“Elimu ndio njia bora ya kuwajengea watoto wetu msingi imara wa maisha yao…serikali haitosita kuchukua hatua za kisheria kwa wazazi au walezi ambao watazembea, kumficha, kumtorosha au kuzuia mtoto kuanza masomo ya shule za msingi na sekondari,” alisema Ummy.

Alisema serikali kupitia Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, itawafungulia mashtaka na kuwapeleka mahakamani wazazi na walezi wote watakaoshindwa kutimiza wajibu wao wa kuwapeleka watoto shule, kwani hata Sheria ya Mtoto Namba 2 ya mwaka 2009 Kifungu cha 8, inaelekeza kuwa ni wajibu wa mzazi kuhakikisha mtoto anapata elimu.

Waziri Ummy alisema Kifungu cha 14 kinatamka kuwa ni kosa la jinai, kushindwa kutimiza wajibu huo na adhabu yake ni faini isiyozidi Sh milioni 5 na kifungo kisichozidi miezi 6; au vyote kwa pamoja.

Alisema pia wazazi na walezi, wahakikishe kuwa watoto wanaoendelea na masomo ya shule ya msingi na sekondari, wanahudhuria masomo yao kwa ufanisi, kwa kuwa serikali haitarajii kuendelea kuona utoro wa watoto shuleni kutokana na sababu zinazoweza kuepukika.

Kuhusu kuwepo kwa mwitikio mkubwa wa watoto wanaoanza masomo, alisisitiza kuwa wazazi, walezi na jamii kuhakikisha kila mtoto mwenye umri wa kuanza elimu ya msingi yaani darasa la kwanza na elimu ya awali, kujiunga na shule kwa muda uliopangwa na kuhudhuria masomo ipasavyo.

Kuhusu kuwepo kwa michango mbalimbali katika baadhi ya shule wakati huu wa maandalizi ya shule, alisema serikali imeshatoa mwongozo stahiki. 
Waziri huyo alisisitiza kwamba sio ada peke yake iliyofutwa, bali hata michango yote na tayari serikali imekwishatoa fedha za kugharimia elimu bure na zimekwishapelekwa katika shule zote nchini.

Kwa ujumla, walimu wakuu hawatakiwi kutoza mchango wa aina yoyote, kama vile ya ulinzi, maji, umeme, uzio, fagio, jembe, ndoo na mingineyo, kwani fedha za kugharimia elimu ya bure zitatumika pia kwenye masuala hayo yote

Mpekuzi blog 
Share:

0 comments:

Post a Comment

MATUKIO MAPYA


Recent Posts Widget

MAKTABA YETU

BLOGS RAFIKI

Powered by Blogger.