TAARIFA YA JESHI LA POLISI KWA VYOMBO VYA HABARI
KUHUSU TAHADHARI KATIKA MKESHA WA MWAKA MPYA
Tunapoelekea
kumaliza mwaka 2015 na kuukaribisha mwaka mpya wa 2016, wananchi
hutumia muda huo kwenda katika nyumba za ibada ama kusherekea katika
maeneo mbalimbali ya starehe, ambapo uzoefu unaonyesha kuwa baadhi ya
watu hupenda kutumia fursa hiyo kufanya vitendo vinavyohatarisha
usalama wa raia mali zao.
Jeshi
la Polisi nchini, limejipanga vizuri katika mikoa yote kwa kushirikiana
na vyombo vingine vya ulinzi na usalama ili kuhakikisha kwamba vitendo
vyovyote vya uhalifu vitakavyojitokeza hususani katika kipindi hiki cha
kuelekea mkesha wa mwaka mpya vinadhibitiwa. Ulinzi umeimarishwa kwenye
maeneo yote ya kuabudia, fukwe za bahari, sehemu za starehe na maeneo
mengine yote ambayo yatakuwa na mikusanyiko mikubwa ya watu.
Aidha,
Jeshi la Polisi linatoa tahadhari kwa wananchi wote kuwa makini na
kuchukua hatua stahiki za haraka kwa kutoa taarifa pindi wanapoona
viashiria vyovyote vya uhalifu katika maeneo yao ya makazi ama maeneo ya
biashara. Simu za polisi endapo mwananchi atakuwa na taarifa ni 111 au
112.
Pia,
Jeshi la Polisi linawatahadharisha wale wote ambao watakuwa wakitumia
barabara kuwa makini na kuzingatia sheria za usalama barabarani na hasa
kwa madereva wa magari na pikipiki, kuepuka kujaza watu kupita kiasi,
kwenda mwendo kasi, kutumia vilevi pamoja na kupiga honi hovyo.
Vilevile,
wananchi kuacha tabia ya kuchoma matairi barabani pamoja na kupiga
mafataki. Aidha, yeyote atakayefanya vitendo hivyo hatua kali za
kisheria zitachukuliwa dhidi yake.
Nawatakieni watanzania wote kheri ya mwaka mpya.
Imetolewa na:
Advera John Bulimba-SSP
Msemaji wa Jeshi la Polisi.
Makao Makuu ya Polisi.
0 comments:
Post a Comment