Mwaka
2016 ni mwaka wa matumaini mapya kwa Watanzania wote walioanza kukata
tamaa ya maisha bora. Biashara nyingi zimefilisika kutokana na vikwazo
mbalimbali.
Familia
nyingi zimeparaganyika kutokana na kukithiri kwa mmomonyoko wa maadili
ya kitaifa na kunyauka kwa utu wa ubinadamu uliochochewa na hali duni ya
maisha miongoni mwa jamii.
Watu masikini na wenye kipato cha chini wameendelea kukosa mtetezi.
Mwaka
2015, wazee wenye umri zaidi ya miaka 65, ambao hawazidi milioni mbili
na nusu hapa nchini, kwa muda mrefu walipaza kilio chao kuhusu haki yao
ya msingi ya kupata ‘mrejesho wa hifadhi ya jamii baada ya kulitumikia
Taifa lao kwa zaidi ya miongo sita, lakini hakuna aliyewasikiliza.
Huduma
za afya ya msingi zilizidi kuwa duni zaidi katika hospitali na vituo
mbalimbali vya afya nchini. Kiwango duni cha elimu na mitalaa
iliyopoteza mwelekeo, ni baadhi ya vizingiti vilivyoikwaza sekta ya
elimu.
Ile
dhana ya kikoloni ya kuwalipa wafanyakazi ujira mdogo au mishahara
kiduchu au ya kiwango cha chini isiyozingatia utu wa binadamu,
iliendelea kukumbatiwa na awamu zilizotangulia.
Kutokana
na haya yote, siyo jambo la ajabu , kuikuta Tanzania ikishika nafasi ya
151 miongoni mwa nchi 170 duniani, kwa kiwango cha chini cha hali ya
ubora wa maisha ya watu wake.
Shirika
la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP) , katika Ripoti yake ya mwaka
2015 , iliyotoa matokeo ya tathmini za utafiti uliofanyika katika nchi
wanachama, ilidhihirisha wazi jinsi ambavyo hata nchi zenye kipato
kikubwa zilivyoshindwa kutumia utajiri wake ili kuboresha hali ya maisha
ya watu wake.
Utafiti huo uliangazia katika maeneo makuu matatu; huduma za afya, ubora wa elimu na viwango vya mapato.
Nchi
nyingi zilizojikuta katika kundi la nchi zenye kiwango cha chini cha
ubora wa hali ya maisha ya watu wake, zilitoka bara la Afrika, baadhi
yake zikiwa na utajiri mkubwa wa maliasili na rasilimali.
Katika
kundi hilo, Kenya ilionekana kuwa na unafuu zaidi kwa kupata kiwango
cha 0.548 (HDI) na kuongoza kundi hilo lenye nchi 44.
Nchi
iliyoshika mkia katika kundi hilo ni Niger, iliyopata kiwango cha 0.348
, ikilinganishwa na viwango vya juu vilivyoshikwa na nchi ya Norway
(HDI 0.944) na Mauritius iliyoongoza katika nchi za bara la Afrika kwa
kiwango cha HDI 0.777.
Ripoti
hiyo inabainisha pia kwamba katika miaka 25 iliyopita, karibu watu
wapatao bilioni mbili kutoka nchi mbalimbali, walifanikiwa kujinasua
kutoka katika kundi la nchi zenye kiwango cha chini cha ubora wa hali ya
maisha.
Tanzania
yenye watu wapatao milioni 45, kuendelea kubaki katika kundi la nchi 44
zenye kiwango cha chini cha ubora wa hali ya maisha ya watu wake, ni
kiashiria cha wazi cha kushindwa kwa sera, mifumo na mikakati yake ya
matumizi sahihi na makini ya maliasili na rasilimali zake
Kwa
mtazamo mwingine ni kwamba, Tanzania ilishindwa kuwa sehemu ya nchi
hizo zenye watu bilioni mbili waliofanikiwa kujinasua kutoka katika
kundi hilo la ubora wa chini.
Mwaka 2016
Kwa nini mwaka 2016 unaweza kuwa Tumaini Jipya na mwanzo mzuri wa safari ndefu ya kiuchumi kwa Tanzania?
Matumaini yote ya Watanzania yapo mikononi mwa uongozi wa Serikali ya awamu ya tano.
Kila
Mtanzania anatarajia labda uongozi huu utakuja na kitu kipya katika
maisha yao, ambacho kilisahaulika kwa miaka mingi. Nacho ni kutokomeza
ufukara na umasikini wa kipato kwa vitendo.
Kama
miaka 25 iliyopita tumeipoteza bila ya kufikia malengo tuliojiwekea,
kutokana na sababu mbalimbali, hatuna sababu tena ya kupoteza miaka
mingine 25 ijayo.
Hata hivyo, uongozi mpya wa awamu ya tano, umeanza kuonyesha dalili njema za kukabiliana na adha hiyo.
Serikali
ya sasa imerithi uchumi ukiwa katika hali duni na tegemezi, huku
taasisi nyingi za umma au za Serikali zikiwa hazifanyi vizuri kama
ilivyo kusudiwa. Rushwa na ufisadi navyo vimetapakaa katika kila nyanja
ya maisha yetu.
Yote
hayo yanafanyika Tanzania ikiwa miongoni mwa nchi chache barani Afrika
zilizobahatika kuwa na utajiri mkubwa wa maliasili na rasilimali
mbalimbali.
Mtu
yeyote aliye na dhamira ya kufunga safari, tena safari ndefu, kwanza
lazima ajue wapi anakotaka kwenda. Akisha jua wapi anakotaka kwenda,
pili, lazima ajue njia atakayopita na namna ya kumfikisha huko
alikokusudia kwenda.
Uongozi
mpya wa awamu ya tano, utalazimika kuangalia nyuma tulikotoka (miaka 25
iliyopita). Kisha utafakari, tunaitaka Tanzania ya aina gani miaka 25
ijayo?
Mpekuzi blog
0 comments:
Post a Comment